Upungufu wa damu kwa wajawazito

0
3946

Mwanamke anapokua na ujauzito maana yake ni kuwa amebeba kiumbe ambacho kinamtegemea yeye kwa kila kitu yaani chakula na hewa safi.

Ili kuweza kufanya vyema kazi ya kusafirisha virutubisho na hewa safi kwenda kwa mtoto aliye tumboni mwili wa mwanamke mjamzito hutengeneza kiasi kikubwa cha damu ili kuweza kufanya kazi vizuri. Ili mwili uweze kutengeneza kiasi kikubwa cha damu huhitaji kiasi kikubwa cha virutubisho muhimu kwa ajili ya utengenezaji huo. Endapo kutakua na upungufu wa virutubisho hivyo muhimu basi damu itakayotengenezwa itakua na upungufu wa vitu muhimu. Wanawake wengi wajawazito huwa na upungufu wa madini ya chuma na virutubisho vingine. Upungufu wa madini chuma hupelekea mwili kushindwa kutengeneza kiasi kinachotakiwa cha chembe nyekundu za damu.

Kushindwa huko kutengeneza kiasi kinachohitajika cha chembe nyekundu za damu ndio husababisha upungufu wa damu unaoonekana kwa wanawake wajawazito wengi Tanzania (na duniani kwa ujumla).

Kuwa na upungufu kidogo wa damu kwa wanawake wajawazito ni jambo linalotegemewa na mara nyingi huwa si jambo la dharura lakini inapotokea upungufu wa damu ukawa mkubwa sana basi hapo ndio huhitajika juhudi za makusudi kufanyika kuweza kurejesha kiwango cha damu katika wingi unaotakiwa

Moja ya changamoto kubwa za kiafya wakati wa ujauzito ni upungufu wa damu. Upungufu wa damu wakati wa ujauzito ni jambo linalotegemewa kutokea mara zote kwa kuwa wakati wa ujauzito mahitaji ya virutubisho mwilini kwa mwanamke aliyekua na ujauzito huongezeka.

Aina za Upungufu wa Damu Wakati wa Ujauzito

Kuna aina tofauti za upunguaji damu wakati wa ujauzito. Tofauti hii ya aina ya upungufu wa damu hutokana na virutubisho gani vilivyopungua/kukosekana na kupelekea kiasi cha damu au ubora wa damu kupungua.

 • Upungufu wa damu kutokana na kupungua kwa vitamin B aina ya Folic acid. Upungufu wa vitamini B aina ya folic Acid husababisha kukosekana kwa malighafi muhimu inayohitajika kutengenezea chembe nyekundu za damu.
 • Upungufu wa damu kutokana na upungufu wa vitamin B 12. Upungufu wa vitamin B12 husababisha pia kukosekana kwa malighafi muhimu inayohitajika kwa ajili ya utengenezaji wa chembe chembe nyekundu za damu.
 • Upungufu wa damu kutokana na upungufu wa madini chuma.

Madini chuma ni muhimu sana kwa uzalishaji wa chembe hai zinazoitwa haemoglobin ambazo kazi yake ni kusafirisha hewa safi. Haemoglobin ni protini inayopatikana ndani ya chembe nyekundu za damu. Upungufu wa madini chuma husababisha upungufu wa protini ya haemoglobin inayofanya kazi ya kusafirisha hewa safi aina ya oksijeni hivyo kusababisha usafirishaji wa hewa hii ya oksijeni kupungua.

Wanawake Wajawazito wa Kundi Lipi Wako Hatarini Kupata Upungufu wa Damu
Wanawake wajawazito wote wako kwenye hatari ya kupata upungufu wa damu mwilini. Hii ni kutokana na sababu niliyoiandika awali kuwa mahitaji ya damu huongezeka wakati wa ujauzito.

Wanawake wajawazito walio kwenye makundi haya wako kwenye hatari zaidi yakupata kiwango kikubwa cha upungufu wa damu;

 • Wale wenye ujauzito wa zaidi ya mtoto mmoja (wenye ujauzito wa mapacha)
 • Wenye changamoto ya kutapika mara kawa mara kuliko kawaida (hali ya kutapika ni moja ya hali za kawaida wakati wa ujauzito hususani wiki 12 za mwanzo wa ujauzito).
 • Waliobeba ujauzito tofauti katika vipindi vya karibu karibu
 • Waliokua tayari na upungufu wa damu wakati wanapata ujauzito.
 • Wasiokula mlo kamili
 • Waliopoteza hamu ya kula kwa kipindi kirefu wakati wa ujauzito
 • Waliobeba ujauzito wakiwa na umri mdogo hususani wale waliobeba ujauzito wakiwa chini ya miaka kumi na tisa (19)

Dalili za Upungufu wa Damu
Upungufu wa damu huanza taratibu hivyo hata dalili zake nazo huanza kidogo kidogo hivyo ni rahisi sana kwa mwenye tatizo kuhisi kuwa ni dalili za kawaida za ujauzito.

Kwa vile wengi hupata upungufu wa damu unaotokana na upungufu wa madini chuma dalili zinazoonekana kwa wingi ni zile zitokanazo na upungufu wa hewa safi kwenye maeneo muhimu ya mwili. Kwa mfano mgonjwa huchoka haraka na kulala sana.

Dalili nyingine ni kama zifuatazo;

 • Ngozi kupauka
 • Midomo kupauka
 • Kusikia kizunguzungu
 • Kushindwa kupumua vizuri
 • Kushindwa kufanya shughuli zinazohitaji kufikiri kwa muda mrefu

Madhara ya Upungufu wa Damu Wakati wa Ujauzito
Madhara ya upungufu wa damu utokanao na upungufu wa madini chuma

 • Kujifungua mtoto mwenye uzito mdogo ukilinganisha na umri wake
 • Kujifungua mtoto mwenye mapungufu kwenye maumbile yake ya mwili
 • Kujifungua mtoto mwenye mtindio wa ubongo
 • Uwezekano wa mama mwenye upungufu wa damu kupata sonona baada ya kujifungua (postpartum depression)

Madhara ya upungufu wa damu utokanao na upungufu wa Folic Acid

 • Mtoto/watoto kuzaliwa kabla ya wakati aliotakiwa/waliotakiwa kuzaliwa
 • Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo ukilinganisha na umri wake
 • Mtoto/watoto kuzaliwa na mapungufu makubwa kwenye mfumo wa fahamu wa kati yaani uti wa mgongo (mfano maradhi ya spina bifida na mengineyo) na ubongo. Mapungufu haya kwa kitaalam huitwa neural tube defects. Mapungufu haya ni makubwa na husababisha watoto kuishi na ulemavu.

Madhara ya upungufu wa damu utokanao na upungufu wa Vitamin B12

 • Mtoto/watoto pia kuzaliwa na mapungufu kwenye mfumo wa fahamu wa kati yaani uti wa mgongo na ubongo.

UPUNGUFU WA DAMU HUGUNDULIKA VIPI?
Mara nyingi ni vigumu kwa mama mjamzito kujua kama ana upungufu wa damu hasa upungufu huo unapokua sio mkubwa mno. Kutokana na ukweli huo wa kutotambua tatizo la upungufu wa damu mapema inashauriwa wanawake wajawazito wawahi kwenda kliniki ya wajawazito ili wafanyiwe vipimo ikiwemo kipimo cha wingi wa damu mwilini.

Vipimo hivi ni muhimu vifanyike mara kwa mara wakati wa ujauzito ili kufahamu kiasi kilichopo cha damu mwilini wakati wote wa ujauzito.

Mara nyingi vipimo vya kiasi cha damu mwilini hufanyika mara moja katika kipindi cha miezi mitatu (wiki 12) ya ujauzito. Yaani hapa namaanisha kipimo cha kwanza hufanyika kati ya mwezi mmoja na wa tatu wa ujauzito, cha pili hufanyika kati ya mwezi wa nne na mwezi wa sita wa ujauzito na kipimo cha tatu hufanyika wakati ujauzito una umri wa miezi saba na miezi tisa.

Matibabu
Wanawake wengi hupata upungufu wa damu wakati wa ujauzito, hivyo ni muhimu kupima mara kwa mara kufahamu wingi wa damu wakiwa wajawazito.

Matibabu yenye lengo la kuongeza kiwango cha damu hutegemea kiwango halisi cha damu iliyopungua mwilini. Kwa Tanzania kuna muongozo maalum wa matibabu kulingana na makundi yafuatayo:

 • Tanzania kama nchi kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii imeweka utaratibu wa kuhakikisha mama wajawazito wanapatiwa Folic acid mapema sana wakati wa ujauzito. Ni muhimu sana kwa wajawazito kuwa na kiasi cha kutosha cha Folic acid mapema kabisa wakati wa ujauzito kwa sababu wiki 3 na ya 4 (mwezi wa kwanza wa ujauzito) ndio mfumo wa fahamu na mifumo mingi mwilini mwa mtoto aliye tumboni huwa inaundwa. Ikitokea mama akawa ana upungufu wa Folic acid wakati ujauzito una wiki tatu (3) mpaka nne (4) kuna uwezekano mkubwa mtoto akaumbwa akiwa na mapungufu kwenye mfumo wake wa kati wa fahamu na hatimaye kuzaliwa akiwa na matatizo ya mfumo wa kati wa fahamu yaani uti wa mgongo (mfano spina bifida) au ubongo.
 • Kwa wale wenye upungufu wa damu wa kawaida usio na madhara yoyote kwa muda mrefu hupewa dawa maalum zenye virutubisho vya madini chuma, vitamin B12 na folic acid ili kusaidia mwili kutengeneza damu ya kutosha. Pia hupewa ushauri wa lishe gani wapate ili waweze kuongeza wingi wa virutubisho muhimu kwa utengenezaji wa damu.
  Kwa wale wenye upungufu wa damu kwa kiwango kikubwa kiasi cha kusababisha madhara makubwa mpaka hata kifo kwa mama mjamzito huwekewa damu moja kwa moja.
 • Kwa wale wenye upungufu mkubwa wa damu lakini usio na dalili yoyote ya kusababisha madhara makubwa au hata kifo lakini waliokaribia sana kujifungua huwekwa kwenye tahadhari maalum inayohusisha uwepo wa damu karibu wakati wa kujifungua kwao au sehemu nyingine hupewa damu kabisa.

LEAVE A REPLY